BRICS yapendekeza mageuzi IMF ili kulinda nchi masikini zaidi
(last modified Sun, 06 Jul 2025 14:35:58 GMT )
Jul 06, 2025 14:35 UTC
  • BRICS yapendekeza mageuzi IMF ili kulinda nchi masikini zaidi

Mawaziri wa Fedha wa nchi wanachama wa kundi la kiuchumi la BRICS la mataifa yanayoendelea wametaka yafanyike mageuzi katika Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF, ikiwa ni pamoja na usambazaji mpya wa haki za kupiga kura na kukomesha utamaduni wa Ulaya kushika usukani wa uendeshaji wa shirika hilo.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na mawaziri hao wa fedha wa kundi hilo baada ya vikao vyao vilivyofanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil ikiwa ni ya kwanza kupitishwa kwa kauli moja na nchi zote wanachama imeunga mkono pendekezo la pamoja la kufanyiwa kazi katika mkutano wa mapitio wa IMF utakaofanyika Desemba mwaka huu, ambao utajadili mabadiliko ya mfumo wa upendeleo ambao unafafanua michango na haki za kupiga kura.

"Urekebishaji wa mgao unapaswa uakisi nafasi za wanachama katika uchumi wa dunia, huku ukilinda hisa za wanachama maskini zaidi," wameeleza mawaziri hao katika taarifa yao ya pamoja baada ya vikao vyao na kuongeza kuwa fomyula mpya inapaswa kuongeza upendeleo kwa nchi zinazoendelea.

Aidha, mawaziri wa BRICS wametoa wito wa kuwepo fomyula mpya yenye uzito wa pato la kiuchumi na uwezo wa kununua, kwa kuzingatia thamani ya sarafu, ambayo inapaswa kuwakilisha vyema nchi za kipato cha chini.

Vikao vya mawaziri hao kabla ya vitafuatiwa na mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi hilo lililopanuka mwaka jana zaidi ya Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini na kujumuisha Misri, Ethiopia, Indonesia, Iran, Saudi Arabia na Muungano wa Falme za Kiarabu.../

OSZAR »